Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani ametawazwa
kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar na kusema
ameshangazwa na mashambulizi ya tindikali dhidi ya viongozi wa dini
Visiwani humo.
Akizungumza na waaandishi wa habari
mara baada ya kutawazwa ndani ya Kanisa la Anglikana la Minara Miwili
Mjini Unguja, Jaji Ramadhan amesema vitendo vya hujuma vinavyofanywa
dhidi ya viongozi wa dini na Serikali ni kinyume na utamaduni wa
Zanzibar.
Alisema Wakristo na Waislamu Zanzibar
kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kama ndugu bila ya kubaguana kwa
sababu za itikadi ya dini licha ya Waislamu kuwa asilimia 95.
Hata hivyo, alikumbusha kuwa wakristo
wana mchango katika harakati za ukombozi wa Zanzibar, ambapo idadi kubwa
ya waumini wake walianzisha Chama cha African Association mwaka 1935,
ambapo rais wake wa kwanza alikuwa hayati, Mzee Augustino Ramadhan na
baadaye akafuata hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Comments