Lilongwe,
Malawi. Mahakama Kuu ya Malawi imepinga uamuzi wa Rais wa nchi hiyo,
Joyce Banda kufuta matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi
ya Malawi (MEC) kwa madai kuwa hana mamlaka hayo.
Mahakama
Kuu ilitoa uamuzi huo jana baada ya Rais Banda kufuta uchaguzi huo kwa
madai kuwa ulikuwa na kasoro, ikiwa ni pamoja na vitendo vya wizi na
matokeo kuchezewa kwenye kompyuta.(Martha Magessa)
Wakati
Rais Banda akitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi alisema: "Ninabatilisha
matokeo ya uchaguzi kwa mamlaka niliyopewa na katiba ya Malawi.
Ninataka kuwapa Wamalawi nafasi nyingine ya kuchangua mgombea anayefaa
kwa uhuru."
Aidha,
Rais Banda alisema kuwa hatagombea tena nafasi ya urais katika uchaguzi
ambao alisema utafanyika ndani ya siku 90 kuanzia sasa.
Awali
mawakili wa serikali ya Malawi, Kalekeni Kaphale, Noel Chalamanda,
Patrick Mpaka waliwasilisha pingamizi mahakamani wakipinga Rais Banda
kufuta matokeo hayo.
Chalamanda
alisema mahakama hiyo imetupilia mbali tangazo la Rais Banda kwa kuwa
hana mamlaka ya kufuta matokeo ya uchaguzi na kusimamisha kazi ya
kuhesabu kura. "Mahakama imesema Rais Banda hana mamlaka ya kufuta
uchaguzi," alisema Chalamanda.
Chalamanda
alisema mahakama hiyo pia imeweka pingamizi Rais Banda kutokana na
hatua yake ya kufuta matokeo na kusimamisha shughuli za kuhesabu kura.
Baada ya
Rais Banda kutangaza kufuta matokeo, hali ya wasiwasi ilitanda katika
mji mdogo wa Limbe ambako polisi wa nchi hiyo walikuwa wakipita huku na
kule wakiwa kwenye magari.
Ulinzi
uliimarishwa juzi katika mji huo baada ya serikali kupata taarifa za
kiintelejensia kwamba raia wa nchi hiyo walipanga kufanya maandamano
kupinga uamuzi wa rais huyo.
Kabla ya serikali kutuma polisi kwenye mji huo, wananchi walianzisha vurugu katika mji mkuu wa Blantyre.
Katika
hatua nyingine, chama cha MCP kimetangaza kwamba mgombea wake, Lazarus
Chakwera ameshinda uchaguzi huo pia tume ya uchaguzi na baadhi ya vyombo
vimekuwa vikishambuliwa kwa kutangaza kuwa mgombea wa Democratic
Progressive Party (DPP) anaongoza kwa asilimia 42.
Kabla ya
Rais Banda kutangaza kufuta matokeo hayo, Tume ya Uchaguzi ya Malawi
(MEC) ilitangaza matokeo ya awali ambayo yalionyesha mgombea wa
Democratic Progressive Party (DPP), Peter Mutharika alikuwa akiongoza
kwa asilimia 42 baada ya kupata kura 683,621 akifuatiwa na Rais Banda
ambaye alipata kura 372,101 sawa na asilimia 23 kupitia People's Party
(PP).
CHANZO:MWANANCHI
Comments