Dar es
Salaam. Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuongoza mkutano wa mashauriano
ya awamu ya kwanza ya uwekezaji katika mradi wa mabasi yaendayo kasi
(DART) utakaowakutanisha wawekezaji wa ndani na nje Dar es Salaam.
Mtendaji
Mkuu wa DART, Asteria Mlambo alisema mwishoni mwa wiki kuwa mkutano huo
utakaofanyika mapema mwezi ujao utatoa nafasi kwa wawekezaji kuzijua
fursa za uwekezaji zitakazopatika kwenye mradi huo.(Martha Magessa)
Washiriki
wa mkutano huo wanatarajiwa kutoka katika benki na taasisi mbalimbali
za kifedha, kampuni za kutengeneza mabasi, kampuni za mawasiliano,
mifuko ya kijamii na wengine.
Mada kuhusu mradi wenyewe wa DART itatolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Jumanne Sagini.
Kabla ya
mkutano huo, DART imeandaa mkutano wa wamiliki wa daladala Dar es
Salaam, Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) na wadau wengine ili
kuwafahamisha jinsi gani wanaweza kunufaika na mfumo huo mpya.
"Tutawaelezea faida na fursa zitakazopatikana kwenye mfumo mpya wa usafirishaji jijini," alisema Mlambo.
Mwezi
uliopita Dart ilikamilisha shughuli ya kusajili mabasi ya daladala
yanayopita katika Barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo
ikiwa ni moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo.
Kulingana
na mpango huo wa Dart barabara hizo za Morogoro, Kawawa na Msimbazi
zitatumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee kwa njia 64 Dar es Salaam
zitakoma kutumika kutokana na mradi huo.
CHANZO:MWANANCHI
Comments