5 Oct 2011
Toleo na 206
Imedhihirika ni jimbo lililo duni kimaendeleo
Hakufanya lolote kubwa kipindi cha ubunge wake KWA takriban miaka mitano, kati ya Oktoba 26, mwaka 1951 hadi Aprili 7, mwaka 1955, Uingereza ilikuwa na Waziri Mkuu aliyeitwa Sir Winston Churchill. Mbali na sifa nyingine za uongozi, alikuwa mpigania ukweli.Katika harakati za kupigania au kutetea ukweli, Sir Winston siku moja alisema: “The truth is incontrovertible. Malice may attack it, ignorance may deride it, but in the end, there it is. Kwamba ingawa ukweli siku zote unaweza kukabiliwa na changamoto nyingi, zikiwamo za uongo, lakini hatimaye hufichuka.Hiki ndicho kilichotokea katika Jimbo la Igunga ambako uchaguzi mdogo wa ubunge umefanyika Oktoba 2, mwaka 2011, kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Rostam Azizi.Rostam amekuwa mbunge wa Igunga kwa takriban miaka 18,kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM). Alichaguliwa kuongoza jimbo hilo kwa miaka mingine mitano katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana (2010).Lakini pamoja na kuchaguliwa tena, alijiuzulu msingi ukiwa ni mchakato wa kujivua gamba ndani ya CCM ambako viongozi wasio waadilifu wanaonyooshewa vidole kwa kashfa za ufisadi, wanapaswa kujiuzulu.Yeye alijiuzulu lakini akidai hizo ni siasa uchwara. Tuache haya ya kujiuzulu kwake kwa sababu sio kiini cha majadala wa leo. Leo nitajadili hali ya jimbo la Igunga katika huduma muhimu na namna haiba ya Rostam Azizi ilivyo katika siasa za kitaifa ili hatimaye turejee kile alichokieleza Sir Winston kuhusu ukweli.Haiba ya Rostam Azizi kitaifa ina taswira nyingi. Ipo taswira ya ufisadi lakini pia ipo taswira ya mwanasiasa mwenye ushawishi au nguvu kubwa ya kisiasa nchini. Nguvu kubwa ya kisiasa na hasa katika Chama cha Mapinduzi (CCM), ushawishi serikalini na tasnia ya biashara.Baadhi ya watu walimpa sifa ya kuwa ndiye mtengeneza viongozi (kings maker) na hasa ushawishi wake kwa viongozi wakuu ambao ndiyo wenye uamuzi wa mwisho wa uteuzi wa nafasi za uongozi.Taswira hizi mbili, kwa hakika, zimejengwa na makundi mawili. Kundi la kwanza ni wanahabari, na hasa wanahabari waandamizi na kundi jingine ni wanasiasa; hasa wale wenye utovu wa kimaadili, wapenda madaraka, wachumia tumbo nk.Kwa sehemu kubwa ujumbe wenye taswira hizo mbili umefikishwa kwenye jamii kupitia wanahabari. Kwa bahati mbaya, wengi wamekuwa wakimwelezea Rostam katika masuala ya kitaifa, iwe kwa ufisadi au ushawishi wake. Ngazi ya ufanisi wake jimboni ilipuuzwa. Na hapa ndipo ninapotaka tutumie busara ya Sir Winston kufichua ukweli.Itakumbukwa kuwa siku ambayo Rostam Azizi alitangaza kujiuzulu ubunge, kuna baadhi ya wakazi wa Igunga waliangua kilio, wengine hawakutaka ajiuzulu. Wakatamka “ bila Rostam hakuna Igunga”.Kwa wale tuliotazama picha za video katika taarifa za habari TBC na kwingineko, pengine miongoni mwetu hasa wasiopenda kudadisi, waliamini ni kiongozi hodari, anayependwa na watu wake, kiasi cha kumlilia. Kwa wale tunaodadisi, tulijiuliza kwa nini wanalia, hatukuishia kuamini eti ni kwa vile anapendwa.Tulijitenga na fikra zilizotolewa na baadhi ya viongozi, akiwamo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye alisema amehuzunika kwa namna watu walivyomlilia Rostam.Lakini kwa wale waliofika katika kampeni za uchaguzi Igunga na kupita katika vijiji vya jimbo hilo na namna huduma za jamii zilivyo Igunga, wengi hasa walioko huru kimawazo, hawataamini kwamba vilio vile vilihusisha maendeleo ya Igunga. Inawezekana vilikuwa vilio vya kukosa baadhi ya misaada binafsi kutoka kwa Rostam.Binafsi, nimefika Igunga katika kufuatilia masuala ya kampeni na mwenendo wa mambo jimboni humo. Nilichokiona ni kwamba kuna pengo kubwa kati ya vilio vya watu wale na umuhimu wa Rostam kwa maendeleo ya Igunga.Wageni waliofika kwenye kampeni Igunga kwa mara ya kwanza bila shaka, wamewahi kujiuliza na hasa wanapotengewa chakula hotelini au kwa mama lishe kama baadhi yetu tulivyokuwa tukiishi kwamba; je, haya maji ni masafi? Na unapouliza hivyo kwa mama lishe unajibiwa “ndiyo maji yetu baba”.Maji ya Igunga kwa wanaofahamu rangi ya chai ya tangawizi ndivyo yalivyo. Hakuna huduma ya maji safi wala salama. Hali hii si kwa vijijini; bali ni katikati ya mji. Kwa kiongozi mwenye haiba ya Rostam kitaifa, hili lilipaswa angalau kutatuliwa kwa hatua.Hali ya vijijini ni balaa tupu. Watu wamefukua mashimo ili kutafuta maji. Hali ni mbaya kwa upande wa huduma ya maji Igunga. Haishangazi, nilipouliza baadhi ya wakazi wa Igunga makazi ya Rostam yako wapi, wakanieleza hakuwahi kuwa na nyumba Igunga!Nilijiuliza mambo mengi kwa nini mtu aliyepigiwa kura halali kwa kuzingatia nguvu za hoja na si fedha, ashindwe kuwa na makazi Igunga? Nilitafakari, ingawa sikuwa na jibu la moja kwa moja. Nilihisi Rostam mwenyewe hawezi kumudu matumizi ya maji ya kiwango duni cha ubora kiasi kile, na hasa kwa kuzingatia haiba yake!Lakini kwa baadhi ya viongozi wa CCM Igunga, inaelezwa kuwa Rostam alikuwa mfadhili wa uhakika wa shughuli za chama na hapo ndipo nguvu zake kisiasa zilipojikita. Amekuwa akitumia fedha binafsi kufadhili vikao vya chama chake, na hata kusaidia shida binafsi za kifedha za viongozi ambao ndiyo mtandao wake wa kumpigia kampeni na ushindi.Nilipowauliza wakazi wa Igunga wanionyeshe makazi ya Rostam, si tu kwamba waliniambia hakuwahi kuwa na nyumba ya kuishi Igunga, lakini pia kuwa hakuwahi kuanzisha mradi wowote binafsi kulingana na uwezo wake kifedha, ili angalau kutoa ajira kwa wana-Igunga na hatimaye kuinua uchumi wa jimbo lake.Hili linajitokeza kutokana na haiba ya Rostam kitaifa kwamba ni mfanyabiashara, mwekezaji. Je, kwa nini hakuwekeza Igunga biashara yenye maslahi kwake na kutoa ajira kwa wana-Igunga? Mbona wafanyabiashara wengine ni wawekezaji Igunga? Inawezekana yapo ambayo Rostam amefanya jimboni Igunga, ikiwamo ongezeko la shule za kata, lakini suala la barabara kuelekea vijijini na huduma ya maji mchango wake ni sawa na hakuna.Je, ni kweli wananchi wanaokosa huduma ya maji safi na salama, kuanzia mjini hadi vijijini wanaweza kuangua kilio kama tulivyoshuhudia alipotangaza kujiuzulu Rostam? Je, walilia kwa maslahi binafsi, wakipuuza maslahi ya wote ambayo ni pamoja na huduma ya maji safi na salama? Mbunge aliyeongoza kwa miaka 18, wakazi wake wakinywa maji yasiyo safi wala salama, wakipita katika barabara za wanyamapori vijijini, alistahili heshima ya kuliliwa? Kwa waliofika Igunga, bila shaka, watakiri wamefichua ukweli kuhusu Rostam.Kwamba, hakufanya au kufanikisha masuala muhimu ambayo yalipaswa kuwa kipaumbele, lakini wengine tukafanye utafiti kuhusu mahudhurio ya Rostam bungeni na hasa katika kutetea watu wake wapate huduma ya maji safi.Amesikika mara ngapi bungeni? Je, mahudhurio yake bungeni yalikuwa ya kuridhisha? Tukijibu maswali hayo, bila shaka tutakuwa tunaielewa falsafa ya Sir Winston kwamba; “The truth is incontrovertible. Malice may attack it, ignorance may deride it, but in the end, there it is.Mungu ibariki Tanzaania, Mungu ibariki Afrika.Chanzo ni Gazeti la Raia Mwema .
Comments