| Send to a friend |
Tuesday, 12 April 2011 22:17 |
WAGENI kutoka nchi jirani ya Kenya wakiwa ndani ya mabasi madogo manne, jana walitinga katika Kijijini Samunge kupata kikombe cha dawa kwa Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT), Ambilikile Mwasapila. Wakenya walianza kuingia kwa wingi kijijini Samunge kuanzia alfajiri na kunywa kikombe dawa inayotolewa na Mwasapila. Sambamba na Wakenya hao, Watanzania wenye asili ya kiasia zaidi ya 30 pia walifika kijijini hapo na walipata kikombe Samunge baada ya kutua na ndege nne za kukodi jana asubuhi. Mkutano wa kijiji leo Samunge Mkutano huo wa kijiji cha Samunge unatarajiwa kufanyika leo wenye ajenda kuu ya mgogoro wa mapato ya ushuru wa magari na helkopta zinazofika huko wakati huu. Mwenyekiti wa Kijiji cha Samunge, Michael Lengume, alisema wananchi wataombwa na Halmashauri ya Kijiji kutoa idhini ya kuanza kukusanya mapato ya Sh2,000 kwa siku kwa kila gari na ndege Sh150,000. Awali, kijiji hicho kilikuwa kikikusanya ushuru huo, lakini baadaye kutokana na maagizo toka Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi, kazi ya kukusanya ushuru iliagizwa kufanywa na halmashauri na gharama zilipanda hadi Sh5,000. Katika gharama hizo, halmashauri itachukuwa Sh2,000 na ofisi za wakuu wa mikoa Sh3,000 kwa kila gari ambapo gharama za helkopta kutua Samunge ni Sh150,000. Diwani wa Kata ya Samunge, Jackon Sandea, alisema jana kuwa wataanza kukusanya ushuru huo kesho kwa kuwa ni haki yao. "Mbona vijiji vingine vinakusanya fedha zao bila shida. Kwa mfano, wageni wanaopanda Mlima Oldonyolengai kijiji kinakusanya fedha, watu waliowekeza vijiji vya Loliondo wanapokea fedha zao, sasa kwa nini wanatuingilia sisi," alihoji Sandea. Alisema fedha za ushuru wa magari ni haki yao, kwani zinasaidia huduma za usafi, ujenzi wa vyoo, masuala ya afya na ulinzi kwa wanaofika Samunge. Uwanja wa ndege Wasso wazidiwa uwezo Uwanja mdogo wa ndege wa Wasso uliopo Loliondo Wilaya ya Ngorongoro, umezidiwa uwezo kutokana na idadi kubwa ya ndege zinazotua kwa siku kupeleka wagonjwa kijiji cha Samunge. Wakizungumza na Mwananchi jana katika uwanja huo, Msimamizi wa Uwanja, Gabriel Masare na Afisa Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Arusha, Fredrick Kimaro, walisema ongezeko la ndege zinazotua hapo ni zaidi ya asilimia 75 ya awali. Masare alisema, awali kabla ya tiba ya Samunge, uwanja huo ulikuwa ukipokea wastani wa ndege moja kwa wiki, lakini sasa ndege kati ya tatu na sita zinatua kila siku. Alisema kutokana na ongezeko hilo, changamoto kadhaa zimeibuka ambazo ni uwanja huo kukosa huduma nyingi muhimu ikiwepo maji, umeme na eneo la kupumzika wasafiri viti na chakula. Kimaro alisema, kwa sasa uwanja huo unapaswa kuwa na umeme kwani baadhi ya ndege hulala hapo. safari za ndege zaanza Samunge Kutokana na idadi kubwa wa wasafiri, makampuni ya ndege ya Coastal Air, Air Excel na ndege ya binafsi ya Babu Sembeke wa Moshi yamenzisha usafiri wa kwenda Samunge. Kwa mujibu wa Kimaro, wastani wa gharama za ndege yenye uwezo wa kubeba watu sita kwenda na kurudi Samunge kwa jumla ya Dola za Marekani2,400. "Kumekuwepo mazungumzo ya kuanzisha safari za ndege kila siku au kwa wiki nadhani muda si mrefu wataanza kwani sasa wanakodiwa na watu kuja hapa,"alisema Kimaro Usafiri wa Helkopta nao washika kasi Usafiri wa helkopta za kukodi toka Jijini, Arusha, mjini Moshi na Jijini Dar es Salaam umeshamiri Samunge kwa sasa. Mwenyekiti wa kijiji cha Samunge, Michael Lengume alisema wastani wa helkopta nne zinatua kwa siku Samunge na wagonjwa mbali mbali. Habari hii imeandikwa katika gazeti la Mwananchi. |
Comments