Waziri wa
Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akitoa hotuba ya uzinduzi
wa Mkutano Mkuu wa kutathmini maendeleo ya sekta ya maji
uliowashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya
nchi. Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa arnautoglo uliopo
maeneo ya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa
Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo wa sekta ya maji walioshiriki
katika Mkutano Mkuu wa kutathmini maendeleo ya sekta hiyo uliofanyika
leo katika ukumbi wa arnautoglo uliopo maeneo ya Mnazi Mmoja, Jijini Dar
es Salaam.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Wizara ya
Maji na Umwagiliaji imejipanga kuanza ujenzi wa mtambo mkubwa wa
majitaka katika maeneo ya Ilala Jijini Dar es Salaam ili kuzuia uchafuzi
wa mazingira nchini.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Mhandisi Gerson Lwenge alipokuwa akizindua Mkutano Mkuu wa kutathmini
maendeleo ya sekta ya maji unaolenga kutatua changamoto zinazozuia
upatikanaji wa maji salama na uondoshaji wa majitaka nchini.
Mhandisi
Lwenge amesema kuwa fedha za mradi huo zimetoka Serikali ya Korea Kusini
ambapo kwa sasa wizara hiyo ipo katika mchakato wa kumtafuta Mhandisi
mshauri ambaye atafanya mapitio sanifu ya manunuzi ya vifaa na baada ya
hapo juhudi za kumtafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mitambo hiyo
zitaendelea.
“Mtambo
huo utajengwa katika wilaya ya Ilala na mabomba yake kutandazwa katika
maeneo yaliyopo katikati ya jiji, Magomeni pamoja na Kurasini ili
kuhakikisha maji machafu yanapata sehemu ya kuelekea na kuacha jiji
likiwa safi siku zote,” alisema Mhandisi Lwenge.
Mhandisi
Lwenge aliongeza kuwa baada ya mtambo huo kukamilika maji
yatakayopatikana yatasafishwa na kutumika kwa matumizi mengine yakiwemo
ya nyumbani, ufugaji, kilimo cha umwagiliaji au kupelekwa moja kwa moja
katika bahari ya Hindi.
Naye
Mwakilishi kutoka Asasi za Kiaraia, Josephine Lemoyan amesema kuwa
uchafuzi wa mazingira unachangiwa na kutokuwa na miundombinu mizuri ya
kupitisha maji machafu hivyo mkutano huo uliofunguliwa leo utajadili
mambo mbalimbali ikiwemo njia za uondoshaji wa majitaka ambayo kwa
kiasi kikubwa unaathiri mazingira yanayotuzunguka.
“Katika
kila sekta mapungufu huwa hayakosekani hivyo kwa kupitia mikutano ya
wadau kama hii inatusaidia kupata mawazo ya kutatua baadhi ya changamoto
zinazozuia uendelevu wa miradi mbalimbali ya majisafi na
majitaka,”alisema Bi. Josephine.
Bi.
Josephine amefafanua kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2016 Tanzania
imejitahidi kuondoa majitaka kwa asilimia 52.6 na ifikapo mwaka 2020
Tanzania inategemewa kufikia asilimia 75 katika suala zima la uondoaji
wa majitaka.
Mkutano
huo wa siku mbili ambao umewashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo
kutoka ndani na nje ya nchi unafanyika katika ukumbi wa arnautoglo
uliopo maeneo ya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.(P.T)
Comments