Katika kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kutekeleza mpango wa
elimu bure, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na viongozi wa vyama vya
usafirishaji abiria jijini Dar es Salaam, wameamua walimu wa shule za
msingi na sekondari kuanzia Machi 7, mwaka huu, kutolipa nauli katika
daladala.
Mpango huo utaanza kutumika baada ya kukamilika utengenezaji wa vitambulisho maalumu kwa waalimu hao wanaokadiriwa kuwa 10,000.
“Ninawatangazia wananchi kuwa kuanzia Machi 7, mwaka huu, walimu wa
sekondari na msingi watasafiri bure katika vyombo vya usafiri katika
jiji letu la Dar es Salaam,” alisema Makonda.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri
Mabruki, alisema makubaliano hayo ni kuunga mkono juhudi za Rais Dk.
Magufuli katika kutekeleza mpango wa elimu bure na kupunguza makali ya
maisha kwa walimu hao.
Alisema walimu wataanza kusafiri bure kuanzia saa 11:30 alfajiri hadi
saa mbili asubuhi, na saa 9 alasiri hadi saa 11 jioni. Nje ya muda
huo, alisema watalazimika kujilipia.
“Tujifunze tunapomuona kiongozi kijana anapopenda maendelea inatubidi
tumuunge mkono. Makonda tangu aingie Kinondoni ameonyesha nia ya dhati
ya kuleta maendeleo,” alisema Mabruki.
Alisema walimu wote watasafirishwa kwa utaratibu wa vitambulisho na kuwapo na utaratibu wa kila gari kuingia walimu wachache.
Chanzo: NIPASHE
Comments