Tangazo hilo la mgawo ambalo limekuja katika kipindi ambacho mjadala wa jenereta za kampuni ya Dowans ukiwa umeibuka tena, linatarajiwa kuongeza gharama za maisha kutokana na ukweli kuwa viwanda vingi vitalazimika kutumia jenereta katika uzalishaji licha ya Tanesco kutangaza kuwa vitapewa umeme nyakati za mchana.
Wananchi ambao kipato chao kinategemea biashara ya samaki, saluni, na vinywaji pia wataguswa na makali hayo moja kwa moja wakati mabenki, vituo vya mafuta, mahoteli na makampuni mengine ya kutoa huduma yatajikuta yakiingia gharama kubwa katika utendaji wao.
Tangazo la Tanesco limetolewa wakati kukiwa na ahadi kemkem za kumaliza kabisa tatizo la mgawo wa umeme, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ikiwa imeliruhusu shirika hilo la umma kuongeza bei ya umeme kwa asilimia 18.5.
"Mgawo huu wa umeme umeshaanza kwenye mikoa yote na utadumu kwa majuma manne hadi katikati ya mwezi Januari mwakani," alisema meneja mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud alipoongea na waandishi jana.
"Mgawo utahusisha mikoa yote iliyounganishwa kwenye gridi ya taifa isipokuwa mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Lindi na Mtwara."
Kwa mujibu wa Masoud, mgawo wa sasa umetokana na upungufu wa umeme uliojitokeza baada ya moja ya visima vinavyozalisha gesi vya kampuni ya Pan African Energy, kuzimwa.
Alisema kisima hicho kinachotoa gesi kimezimwa kwa ajili ya kukifanyia matengenezo ya kawaida, hivyo kusababisha upungufu wa megawati 40 za umeme zinazokwenda katika gridi ya taifa.
Pan African Energy ni kampuni ambayo inachimba gesi hiyo eneo la Songo Songo, Kilwa na baadaye husafishwa na kusafirishwa na kampuni ya Songas ambayo huzalisha umeme wa megawati 180 eneo la Ubungo na kuiuzia Tanesco.
Kwa mujibu wa makubaliano, Songas hutakiwa kuzalisha umeme kwa kiwango kilicho kwenye mkataba na ni jukumu la Tanesco kuutumia umeme huo wa gesi kulingana na mahitaji yake au kutoutumia. Tanesco huilipa Songas hata pale inapokuwa haitumii umeme wa kampuni hiyo.
Badra alisema kuwa kiwango hicho cha upungufu wa umeme kinaweza kuongezeka hadi kufikia megawati 120 jambo alilosema likitokea, shirikma hilo litazidisha mgawo.
“Wakati mwingine kunapokuwa na peak (matumizi yanakuwa makubwa), upungufu unaweza kufikia megawati 120. Ikitokea hivyo, kwa kuwa sasa tunategemea uzalishaji umeme kwa njia ya maji, itabidi nasi tuongeze mgawo,” alisema Badra.
Alieleza kuwa mgawo huo utaanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni katika baadhi ya maeneo huku maeneo yaliyopata umeme katika muda huo yakiukosa kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 5:00 usiku mara tatu kwa wiki.
Kwa mujibu wa Badra, ratiba ya mgawo huo zitatangazwa katika magazeti na vyombo vingine vya habari.
Hata hivyo, alisema baadhi ya maeneo hayatakumbwa na mgawo huo akitaja baadhi kuwa ni hospitali, pampu za maji, migodi na viwandani ambako alisema vitakosa umeme usiku ili mchana viendelee kuzalisha.
Alisema kuwa maeneo yanayopata umeme kutoka transoma ya Kipawa hawatakumbwa na mgawo huo, kutokana na kukamilika kwa matengenezo yake.
“Transfoma ya Kipawa imeshatengemaa na hivyo kuanzia Desemba 23 (jana) haki ya kupata umeme katika maeneo yaliyoathirika kutokana na kuharibika kwa transfoma hiyo, itarejea kama kawaida na wateja wa maeneo hayo hawatakumbwa na mgawo huu tulioutangaza,” alisema Badra.
Baadhi ya maeneo yanayopata umeme kutoka transfoma hilo ni pamoja na Yombo Dovya, Tandika, Temeke, Chang’ombe, Chamazi, Tazara, Maji Matitu, Charambe, Keko na Uwanja wa Taifa.
Akizungumzia siku kuu za Krisimasi na Mwaka Mpya, Badra alisema Tanesco itajitahidi kuhakikisha wananchi wanasherehekea siku hizo bila kukosa umeme huku akiwaomba radhi kwa mgawo huo.
Mgawo wa umeme, ambao ulizalisha kashfa kubwa ya Richmond ulipoibuka mwaka 2006, umeshaanza kuzoeleka kwa wananchi na ahadi za shirika hilo na wizara kugeuza tatizo hilo kuwa historia, sasa zinaonekana za kawaida.
Machi 16 mwaka huu Tanesco ilitangaza mgawo wa umeme katika mikoa yote ya Tanzania Bara uliokuwa wa saa tano kila siku. Wakati mgawo huo ukiisha, Tanesco ilitangaza kuwa tatizo la umeme sasa litakuwa historia.
Watanzania, ambao ni asilimia 12 tu wanaotumia huduma hiyo majumbani, pia walipata machungu ya mgawo wa umeme Oktoba mwaka uliopita ambapo walikosa huduma hiyo kwa saa 12 kwa siku.
Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo Stephen Mabada, alitangaza mgawo huo akieleza kwamba Tanesco ililazimika kuanza mgawo huo kutokana na upungufu mkubwa wa uzalishaji umeme, uliosababishwa na kuharibika kwa mitambo minne kwenye vituo vya uzalishaji wa nishati hiyo.
Mitambo iliyoharibika ilikuwa ni ya Kidatu, mkoani Morogoro, Kihansi (Iringa) na Pangani (Tanga) wakati jijini Dar es Salaam mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi asilia wa Songas pia uliripotiwa kuharibika.
Wakati huo, serikali iliamuru kuwashwa kwa mitambo inayozalisha umeme kwa kutumia mafuta ya IPTL licha ya kampuni hiyo na Tanesco kuwa kwenye mgogoro mkubwa ambao unashughulikiwa mahakamani.
Matatizo makubwa ya umeme yaliibuka mwaka 2006 wakati nchi ilipokumbwa na janga kubwa la ukame na ikabidi serikali ichukue hatua za dharura kumaliza tatizo hilo.
Lakini hatua hizo za dharura zikaishia kwenye kashfa kubwa ya utoaji zabuni ya uzalishaji umeme kwa kampuni ya Richmond Development LLC, ambayo ilidhihirika baadaye kuwa haikuwa na uwezo wa kutekeleza wajibu wake kwenye mkataba.
Baadaye mkataba huo ulirithishwa kwa kampuni ya Dowans Tanzania ambayo, licha ya kuchelewa, ilileta nchini mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi iliyokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 120.
Lakini mwaka 2008 Tanesco ilikatisha mkataba huo mwaka mmoja kabla ya kumalizika, ikidai kuwa Sheria ya Manunuzi ya Umma ilikiukwa wakati wa kuingia mkataba huo, lakini ikaahidi kuwa ina uwezo wa kuzalisha umeme bila ya kutegemea jenereta hizo.
Uamuzi huo uliifanya Dowans kufungua kesi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC), ikidai kuwa taratibu hazikufuatwa wakati wa kuvunja mkataba huo.
Mwaka mmoja baadaye Tanesco ikaibuka na hoja ya kutaka kuinunua mitambo hiyo ya Dowans, ikidai kuwa nchi ilikuwa hatarini kuingia kwenye tatizo kubwa la umeme na kwamba isingekuwa rahisi kununua mitambo mingine kabla ya tatizo hilo kuanza.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa vikali na Kamati ya Madini na Nishati ambayo ilieleza kuwa kununua mitambo hiyo mitumba ni kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma, kitu kilichomfanya mkurugenzi wa Tanesco wa wakati huo, Dk Idris Rashid kutoa tamko kuwa iwapo nchi itaingia gizani, asilaumiwe.
Mapema mwezi huu, ICC) ilitoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Dowans na kuiamuru Tanesco kuilipa kampuni hiyo binafsi fidia ya Sh185 bilioni.
Source: www.mwananchi.co.tz
Comments