Aliyekuwa mgombea Ubunge wa jimbo la Morogoro
mjini kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Suleman Msindi alimaarufu
kama 'Afande Sele' amefunguka na kusema hawezi kufanya muziki tena, na
badala yake atajikita katika shughuli za kilimo.
Afande
Sele amesema haya katika kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio
na kudai sasa atafanya kilimo pamoja na ufugaji na maamuzi haya
yamekuja kutokana na yeye kushindwa katika uchaguzi wa mwaka huu, na
ameamua iwe hivyo kwa sababu tayari anaamini amepoteza mashabiki wake
wengi ambao walikuwa Ukawa na CCM ambao walikuwa wanaamini katika maono
na mashairi yake.
“Kwa sasa nimeamua tu kufanya kilimo pamoja ufugaji sitafanya muziki
tena sababu nilipoingia kwenye siasa mlango nilioingilia huu wa
ACT-Wazalendo umenifanya niwaache mashabiki zangu wengi Ukawa na CCM
hivyo sidhani kama wanaweza kunielewa tena sababu watu walikuwa
wakipenda kazi zangu kutokana na maono na ubora wa mashairi hivyo
wanaweza wasiniamini sababu ya kuingia upande ambao hawakuutarajia
kabisaa,” alisema Afande Sele.
Amesema kuwa uchaguzi wa mwaka huu kupitia chama chao cha
ACT-Wazalendo hawakufanya vizuri kwa sababu ndio kwanza walikuwa
wanakijenga chama hivyo hawakuwa na ushindani, ila anaamini mwaka 2020
watanzania watawaelewa zaidi maana watakuwa wameshajua upi mchele na ipi
pumba.
Hata hivyo Afande Sele ameongeza kuwa kama ni muziki atafanya muziki
kwa burudani sababu ni msanii ila si kufanya muziki kazi kama ilivyokuwa
awali.
Comments