Dar es Salaam. Emmanuel Mbasha, ambaye ni mume wa mwimbaji nguli wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha amejitokeza hadharani na kusema kwamba atakwenda polisi mwenyewe kujibu tuhuma dhidi yake za kumbaka shemeji yake mwenye umri wa miaka 17.
Faili la tuhuma dhidi ya Mbasha lilifunguliwa Jumatatu iliyopita katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule) wakati shemejiye huyo (jina tunalihifadhi), alipotaarifu kuwa Mbasha alimbaka mara tatu kwa siku mbili tofauti. Kesi hiyo ilipewa namba TBT/RB/3191/2014 na TBT/IR/1865/2014.
Tangu siku hiyo, polisi imekuwa
ikieleza kuwa inamsaka Mbasha bila ya mafanikio lakini mwishoni mwa wiki
mtuhumiwa huyo aliongea na gazeti hili na kuelezea upande wake wa tukio
hilo na kwamba yuko tayari kujisalimisha ili ukweli ubainike.
"Tuhuma dhidi yangu ni za
kutengeneza," alisema Mbasha na kufafanua kuwa yote hayo yanatokana na
mgogoro wa kifamilia baina yake na Flora na familia yake ambao alisema
umedumu kwa siku kadhaa.
"Mimi sijabaka na sijawahi kubaka;
sijatenda dhambi yoyote; sijafanya kitu chochote na kibaya haya mambo
yote ni ya kusingiziwa tu. Mungu wangu ni shahidi. Na kwa kuwa sijafanya
hiyo dhambi kama wanavyodai, basi Mungu wangu atanitetea," alisema
Mbasha ambaye anaonekana zaidi kwenye video ya wimbo wa Maisha ya Ndoa
alioshirikiana na mkewe Flora.
"Si wamesema wananitafuta, nitakwenda
mwenyewe polisi. Nitawasikiliza na nitatoa maelezo yangu. Kama
wakinipeleka mahakamani basi ukweli utajulikana... ipo siku kila kitu
kitakuwa wazi."
Kabla ya kufunguliwa kwa faili la
tuhuma hizo, msichana huyo alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya
Ilala (Amana) ambako alifunguliwa faili la matibabu namba 667. Matokeo
ya vipimo ambavyo vilifanywa na daktari kung'amua kama binti huyo
aliingiliwa vinaonyesha kuwa kulikuwa na mbegu utokaji wa mbegu usio wa
kawaida (HVD).
Kadhalika binti huyo alifanyiwa vipimo
kuona kama ameambukizwa virusi vya Ukimwi (VVU), pia kupata ujauzito,
lakini matokeo ya awali yalionyesha kuwa yupo salama.
Akiwa nje ya kituo cha polisi Jumatatu
usiku, binti huyo aliliambia gazeti hili kwamba mara ya kwanza alibakwa
mchana Mei 23 na kwamba mtuhumiwa alirudia kitendo hicho Jumapili Mei
25 usiku ndani ya gari katika eneo la Tabata, ambako anadai alifanyiwa
kitendo hicho mara mbili.
Hata hivyo, Mbasha alihoji: "Hivi
kweli hata kama mimi ni mbakaji, kweli nimbake mtoto wa kumlea mwenyewe
mara tatu, yaani Ijumaa halafu nirudie tena Jumapili? Hata kama ni
kusingiziwa basi tuhuma hizi zimezidi."
"Huyu binti nimekaa naye miaka mingi
na sijawahi kumfanyia hivyo. Hapo nyumbani kwangu wamekaa mabinti wengi,
wakiwamo shemeji zangu wadogo zake na Flora na sikuwahi hata kuwagusa,
leo hii kwa nini wananifanyia hivi?"
Mbasha alidai kwamba chanzo cha
kusingiziwa kwake ni mgogoro baina yake na mkewe Flora, ambao
umesababisha mgawanyiko mkubwa ambao umefanya achukiwe na familia nzima
ya mkewe.
"Yako mambo mengi tu ambayo yanahusu
familia, kwa hiyo ilifika mahali mimi na Flora tukawa hatuishi kwa amani
na hata hili jambo limetokea wakati tukiwa na mgogoro huo. Hivyo Flora
na ndugu zake waliamua kumlisha binti huyo maneno ili mimi nifungwe,"
alisema Mbasha.
Hata hivyo, Flora hakutaka kuingia kwa
undani katika suala hilo, akisisitiza kuwa Mbasha bado ni mumewe na
kwamba yaliyotokea awali alishamsamehe, lakini akamtaka ajitokeze kutoa
maelezo polisi.
"Mimi nilishamwambia kwamba hata kama
alifanya au hakufanya, nilishamsamehe kutoka ndani ya moyo wangu maana
yeye ni mume wangu wa ndoa na Mungu wangu ni shahidi, lakini kuna suala
la kisheria polisi ambalo mimi siwezi kuliingilia," alisema Flora ambaye
alitamba na wimbo wa injili wa "Tanzania" ambao ulimfanya aalikwe
katika shughuli mbalimba za kitaifa.
"Tatizo linakuwa kubwa kwa sababu yeye
mwenyewe haonekani na taarifa ni kwamba amekimbia," alidai Flora. "Sasa
kama kweli hajafanya kitendo hicho, kwa nini anajificha? Ajitokeze...
aende polisi na huko ndiko akatoe maelezo yake. Kuzungumza na vyombo vya
habari haisaidii kabisa."
Mwimbaji huyo, ambaye ni mjukuuu wa
muhibiri maarufu wa Injili, Askofu Moses Kulola alisema yeye hana uwezo
wa kuingilia kesi hiyo kwani hakuhusika kwa namna yoyote ile kupeleka
suala hilo polisi kwa sababu hakuwapo wakati likitokea na kwamba
linasimamiwa na familia.
"Inawezekana anatamani nikafute kesi
polisi, mimi sina uwezo huo kwa sababu ni suala la kisheria na tuhuma
zenyewe ni za kijinai. Pili familia yenye mtoto ndiyo inafuatilia kesi
hiyo, lakini hilo halifuti msamaha wangu kwake," alisisitiza.
Kauli ya Flora kwamba ameshamsamehe
mumewe inafanana na ya Mbasha ambaye pia alisema kwamba kama kuna jambo
ambalo mkewe alimkosea, hana tatizo na kwamba alishamsamehe.
"Flora ni mke wangu, mke wa ujana
wangu, ninampenda asilimia 100 na yeye analifahamu hilo, lakini sijui ni
kitu gani kimemkuta? Sijui ni nini kimeingilia ndoa yetu?" alisema
Mbasha.
Alisema ameshampigia simu mkewe mara
nne akitaka waonane ili wazungumze, lakini hakuonyesha utayari, kauli
ambayo Flora aliikanusha akisema: "Hajanitafuta maana tangu Jumatatu
hapatikani kwenye simu."
Mwenendo wa upelelezi
Wakati hayo yakiendelea, maendeleon ya
kesi hiyo yanasuasua baada ya faili kutokupelekwa Kituo cha Polisi
Buguruni kutoka Tabata kwa ajili ya hatua zaidi.
Baadhi ya wanafamilia wa mtoto
anayedaiwa kubakwa walisema jalada hilo lingefikishwa Buguruni Jumatano
jioni, lakini kutokana na ofisa anayeshughulikia kesi hiyo kuwa na
udhuru, ilishindikana.
Mjomba wa Flora ambaye amepewa jukumu
la kusimamia kesi hiyo, alisema wamekuwa wakifuatilia Kituo cha Polisi
cha Tabata tangu tukio hilo liliporipotiwa, lakini wakaelezwa kuwa kesi
hiyo itahamishiwa Buguruni.
"Tuliambiwa lile faili lazima lihamie
kituo cha Buguruni. Nilifika hapa nikaonana na kamanda wa polisi wa
wilaya ambaye ametupokea vizuri na kuonyesha moyo wa kutusaidia,"
alisema.
Kamanda wa polisi wa Ilala, Marietha
Minangi alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa kesi hiyo na kwamba
hafahamu taarifa kuwa faili hilo linacheleweshwa kuhamishiwa Buguruni.
"Tunaendelea kuchunguza, ila siyajui hayo masuala ya faili yanayotoka
kinywani mwako. Lakini nimepata taarifa kuwa bado wanachunguza," alisema
Minangi.
Mwanzoni mwa wiki jana, Kamanda
Minangi alisema kuwa maofisa wake walikuwa wanaendelea kumsaka mtuhumiwa
na kwamba walienda mpaka nyumbani kwake, lakini hawakumkuta.
"Nimefuatilia ni kweli hiyo kesi
imefunguliwa na maofisa wangu wameniambia walienda nyumbani kwake na
hawakumkuta mtu. Waliniambia walikaa pale kwa takribani dakika 20 na ile
nyumba ina fence (uzio) na geti waligonga kengele, lakini hakuna mtu
aliyekuja kufungua.
"Na baadaye waliwauliza majirani, nao
wakasema hawafahamu mtu huyo alipo. Inaonekana ametoweka, lakini sisi
kama wasimamizi wa sheria tunaendelea kumtafuta mpaka tutakapomkamata,"
alisema Minangi.
Ustawi wa Jamii
Kesi hiyo pia inafuatiliwa kwa karibu
na Idara ya Ustawi wa Jamii ya Manispaa ya Ilala kujua usalama na
matibabu ya binti huyo. Ofisa ustawi wa jamii anayeshughulikia ulinzi na
usalama kwa mtoto wa manispaa hiyo, Fransica Makoye alisema kuwa
wanalishughulikia suala hilo kama mengine katika kutafuta haki na
usalama wa mtoto na wala hawahusishi na umaarufu wa wahusika.
"Sisi tunafuatilia kama alipata tiba
sahihi mara baada ya tukio la kubakwa na kufahamu mahali ambako anakaa
kwa ajili ya usalama wa huyo mtoto. Tumeiona PF3 haionyeshi kama alipata
matibabu, lakini tutawajulisha zaidi kinachojiri kwa kuwa tutaenda
Hospitali ya Amana kwa maelezo zaidi," alisema Makoye.(E.L) Chanzo ni www.mjengwablog.com
Comments